07 January, 2007

ONGEZEKO LA WATOTO WAMITAANI (TANZANIA)

Tanzania ni miongoni mwa nchi za kiafrika zilizo masikini sana. Kwa kiasi fulani imefanikiwa kutatua sehemu ya matatizo hasa tatizo la ujinga kwa kufuta gharama za elimu ya msingi na kuhakikisha kila mtoto anaandikishwa darasa la kwanza. Lakini, pamoja na juhudi hizo, bado kuna matatizo ambayo yanaibuka kama uyoga, mfano wa hayo ni rushwa, ukosefu wa ajira na ongezeko la watoto wa mitaani. Zifuatazo hapa chini ni sababu kuu muhimu ambazo zinasababisha ongezeko la watoto wa mitaani;
Kuzaa watoto wengi, kwa baadhi ya jamii nchini Tanzania bado zinaamini kuwa na watoto wengi ni heshima na fahari kubwa. Hivyo zinazaa watoto wengi na matokeo yake wanashindwa kuwapatia huduma muhimu kama vile afya na elimu. Baadae hao watoto huamua kukimbilia mjini wakiwa na matumaini ya kupata kazi na maisha mazuri. Wanapokikosa kile wanachokitegemea ndipo wanajikuta mitaani.

Umasikini uliokithiri katika familia humfanya mtoto aondoke nyumbani na kwenda mjini kwa ajili ya kutafuta maisha. Na kwasababu mtoto huyo hajasoma anaishia kuuza maji tu, biashara mbayo haiwezi kukidhi mahitaji yake ya kila siku. Mtoto wa namna hii ataanza kutumia madawa ya kulevya kwa madai ya kujifariji na hatimaye kuongeza idadi ya watoto wa mitaani.
Elimu ya uzazi, kuna baadhi ya jamii huko vijjini na hata mjini bado hazina elimu ya kutosha juu ya uzazi . Hii husababishwa na mimba zisizotarajiwa, na mtoto anapozaliwa hukosa huduma muhimu matokeo yake mtoto huyu huishia mitaani.

Vifo, kutengana, au wazazi kufariki kwa ajali au magonjwa kama vile HIV/ AIDS na kuwaacha watoto wadogo. Hao yatima kama hawakutunzwa na ndugu au chombo chochote kinachojihusisha na watoto, wataishia kuwa watoto wa mitaani.

Ili kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani, jamii yenyewe ni lazima ikubali mabadiliko kwa kufuata uzazi wa mpango. Yaani kuzaa watoto ambao familia inauwezo wa kuwatunza . Pia mashirika yasiyo ya kiserikali yaani NGOs yawepo angalau katika kila mkoa kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye matatizo hayo badala kun'gan'gania mkoa mmoja wa Dar es salaam. Na mwisho ,serikali ingetupia jicho hasa vijijini na kuendesha semina juu ya uzazi wa mpango na madhara ya ngono holela. Hii inaweza kupunguza ongezeko la watoto mitaani.

Shukrani.

Anna komba.

January 07, 2007







4 comments:

Simon Kitururu said...

Hili tatizo la watoto wa mitaani ni gumu sana.Kazi tunayo!

Egidio Ndabagoye said...

Karibu sana dada'ngu.hapa naona kutakuwa na vitu vya uhakika.

Anonymous said...

Msangi Mdogo kanipa taarifa ya blogu yako. Karibu ulingoni. Tuko pamoja.

Jeff Msangi said...

Karibu sana kwenye ulimwengu huu wa blog.Jitahidi kuandika mara kwa mara.