14 February, 2007

NINI KINACHOWAFANYA WATU WAZAE IDADI FULANI YA WATOTO? JE NI UFAHARI, HULKA, DOLA, DINI AU UWEZO WA KIFEDHA?

Labda ndugu msomaji jiulize swali hilo. Kiasi cha majuma mwezi mmoja hivi uliyopita
nilionyesha jinsi gani kunakuwa na ongezeko la watoto wa mitaani. Na leo bado jicho langu limejikita zaidi mitaani na kuzimulika familia tofauti katika pande kuu nne za dunia.

China ni moja kati ya mataifa makubwa barani Asia na dunia kwa ujumla. Inakadiriwa kuwa na robo ya watu wote duniani, ambayo ni watu bilioni moja na nusu. Idadi hiyo ya watu, labda ingekuwa zaidi ya hapo kama serikali (dola) ya nchi hiyo isingeweka idadi ya mtoto mmja katika kila mwanandoa. Hivyo, wananchi wa china wanazaa watoto kulingana na agizo la dola nasio wanavyotaka wao!
Swala hilo nitofauti sana katika nchi nyingi za kiafrika mfano Tanzania, ambapo unaweza kuona familia moja ina karibu watoto sita, saba mpaka nane! Watoto hao huzaliwa kama ndege kwenye kiota na pindi wanapokuwa na kuota mabawa huruka huku na kule pasipokuzingatia suala la elimu au afya. Baadhi ya familia hizo huona fahari kubwa kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto. Kama inavyofahamika bara la Afrika ndilo masikini zaidi duniani, lakini linaongoza kwa kuwa na kiwango cha juu katika kuzaa watoto. Matokeo yake ni kushindwa kuwapa watoto hao huduma kama vile SHULE na AFYA. Heeh! Watanzania wenzangu na Waafrika kwa ujumla amkeni! achaneni na dhana inayowaumiza. Mda umefika kwenda pamoja na mabadiliko ya dunia, tuachane na utaratibu au mazoea ya kale, tutakufa MASIKINI!?

Hebu tuliangalie bara la Ulaya, ambalo ndilo bara tajiri zaidi duniani. Chakushangaza zaidi hapa ni kwamba, idadi ya watu katika bara lote Ulaya haifikii ile ya nchi ya china! Hapa tunajifunza nini? Ikiwa Uingereza wana uwezo wa kiuchumi , mbona hawazaliani kama ilivyo kwa Tanzania? Si wazaliane tu kwa wingi, kwa kuwa wao wana uwezo wakuwatunza watoto wao? Je nchi hizi za Ulaya zinzingatia nini? Mbona zinakumbwa na uhaba wa wafanyakazi hata kudiriki kuwaingiza wafanyakazi toka nchi nyingine ?

Katika baadhi ya vitabu vya dini vimesisistiza kwamba, watu wakazaline na kuijaza dunia, na baadhi ya wanadini huoa wake zaidi ya mmoja jambo ambalo linatoa nafasi ya kuwa na watoto wengi katika familia na hatimaye nchi kwa ujumla.

Ndugu msomaji , uwanja ni wako, fungua masikio na macho yako tafuta pa kuegemea!

07 January, 2007

ONGEZEKO LA WATOTO WAMITAANI (TANZANIA)

Tanzania ni miongoni mwa nchi za kiafrika zilizo masikini sana. Kwa kiasi fulani imefanikiwa kutatua sehemu ya matatizo hasa tatizo la ujinga kwa kufuta gharama za elimu ya msingi na kuhakikisha kila mtoto anaandikishwa darasa la kwanza. Lakini, pamoja na juhudi hizo, bado kuna matatizo ambayo yanaibuka kama uyoga, mfano wa hayo ni rushwa, ukosefu wa ajira na ongezeko la watoto wa mitaani. Zifuatazo hapa chini ni sababu kuu muhimu ambazo zinasababisha ongezeko la watoto wa mitaani;
Kuzaa watoto wengi, kwa baadhi ya jamii nchini Tanzania bado zinaamini kuwa na watoto wengi ni heshima na fahari kubwa. Hivyo zinazaa watoto wengi na matokeo yake wanashindwa kuwapatia huduma muhimu kama vile afya na elimu. Baadae hao watoto huamua kukimbilia mjini wakiwa na matumaini ya kupata kazi na maisha mazuri. Wanapokikosa kile wanachokitegemea ndipo wanajikuta mitaani.

Umasikini uliokithiri katika familia humfanya mtoto aondoke nyumbani na kwenda mjini kwa ajili ya kutafuta maisha. Na kwasababu mtoto huyo hajasoma anaishia kuuza maji tu, biashara mbayo haiwezi kukidhi mahitaji yake ya kila siku. Mtoto wa namna hii ataanza kutumia madawa ya kulevya kwa madai ya kujifariji na hatimaye kuongeza idadi ya watoto wa mitaani.
Elimu ya uzazi, kuna baadhi ya jamii huko vijjini na hata mjini bado hazina elimu ya kutosha juu ya uzazi . Hii husababishwa na mimba zisizotarajiwa, na mtoto anapozaliwa hukosa huduma muhimu matokeo yake mtoto huyu huishia mitaani.

Vifo, kutengana, au wazazi kufariki kwa ajali au magonjwa kama vile HIV/ AIDS na kuwaacha watoto wadogo. Hao yatima kama hawakutunzwa na ndugu au chombo chochote kinachojihusisha na watoto, wataishia kuwa watoto wa mitaani.

Ili kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani, jamii yenyewe ni lazima ikubali mabadiliko kwa kufuata uzazi wa mpango. Yaani kuzaa watoto ambao familia inauwezo wa kuwatunza . Pia mashirika yasiyo ya kiserikali yaani NGOs yawepo angalau katika kila mkoa kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye matatizo hayo badala kun'gan'gania mkoa mmoja wa Dar es salaam. Na mwisho ,serikali ingetupia jicho hasa vijijini na kuendesha semina juu ya uzazi wa mpango na madhara ya ngono holela. Hii inaweza kupunguza ongezeko la watoto mitaani.

Shukrani.

Anna komba.

January 07, 2007







03 January, 2007

HERI YA MWAKA MPYA

Nawatia mwaka mpya wasomaji wangu.

Hodi Hodi Mtandaoni

Shukrani za pekee kwa rafiki yangu msangimdogo mwenye kumiliki blogi za msangimdogo na fikiri kwa ushawishi wake mkubwa na msaada wake mkubwa katika kufanikisha mimi kujiunga na Jumuiya ya waandishi wa mtandaoni wa kitanzania. Ningali mchanga sana hivyo natarajia msaada mkubwa kwenu nyote katika kunifikisha mbali zaidi kwenye kuielimisha jamii.

Nabisha hodi nikitarajia hamtakuwa wachoyo mtanikaribisha.